Saturday, June 8, 2013

Taifa Stars yazimiwa taa ikifanya mazoezi nchini Morocco soma hapa jinsi ilivokuwa


Timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars jana usiku ilifanyiwa kilichoonekana kuwa hujuma baada ya kufanyiwa vurugu na kuzimiwa taa ishindwe kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Marrakech nchini Morocco. Stars ilikuwa ikifanya mazoezi ya mwisho mwisho kabla ya mchezo wao dhidi ya wenyeji Morocco leo, kuwania tiketi ya kucheza fainali za kombe la dunia.





Sheria za FIFA zinasema timu ngeni, itapewa fursa ya kufanya mazoezi katika uwanja utakaotumika kwa mechi dhidi ya wenyeji katika muda ambao mechi itachezwa, lakini jana msafara wa Stars ulipofika uwanja wa Marakech ulizuiwa kuingia ndani na askari wa uwanjani hapo.

Juhudi za kocha mkuu wa Stars, Kim Poulsen kuwaelewesha askari wa uwanja huo kuhusu sheria hiyo ili wairuhusu timu kuingia uwanjani hazikuzaa matunda na ikabidi viongozi wa shirikisho la soka Tanzania (TFF) waingilie kati ambao nao pia wakachemsha.



Ikawadia zamu ya viongozi wa kamati ya ushindi ya Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premum Lager, ambao nao walichemsha,ndipo baadhi wa Watanzania waishio Morocco na wachache waliosafiri kutoka Dar es Salaam walipoongeza nguvu.

Walikwenda kufungua geti kwa nguvu, wakawaweka kando askari waliokuwa wanawazuia na kuiingiza timu uwanjani kufanya mazoezi.



Hata hivyo, Stars ilipofika uwanjani ililazimika kusubiri tena, kwani wenyeji Simba wa Atlasi walikuwa wakiendelea na mazoezi.

Baada ya nusu saa, Morocco walimaliza awamu yao na Stars wakaanza kupasha misuli moto. Hata hivyo, baada ya dakika 34, taa za Uwanja huo zilizimwa na uwanjani kuwa giza totoro, lakini viongozi wa TFF wakaenda kuomba, zikawashwa na timu ikafanya mazoezi kwa dakika 10 zaidi.



Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Mh. Amos Makalla aliyekuwapo wakati wa vurumai zote hizo, alisikitishwa mno na kitendo hicho akisema si cha kiungwana na si cha kiunamichezo. Makamu wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani alisema Morocco walikuja kucheza Dar es Salaam walipokelewa vizuri na wakahudumiwa vizuri hadi wanaondoka, ajabu leo wanaifanyia ‘unyama’ Tanzania.







Source: Kilimanjaro Premium Lager (Facebook). Picha: Bin Zubery

0 comments:

Post a Comment