Monday, June 15, 2015

LIPUMBA awashangaa wanaostahili jela kuchukua fomu za Urais na Muhimbili yakaukiwa damu..#MAGAZETINI JUNE 15


HERE
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amechukua fomu ya kugombea urais kupitia chama hicho na kuahidi kupambana na rushwa huku akishangaa kuwapo watuhumiwa wa ufisadi waliotakiwa kuwa mahabusu lakini wakichukua fomu za kuwania nafasi hiyo kupitia CCM.
Profesa Lipumba alisema iwapo atapatiwa ridhaa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupeperusha bendera ya umoja huo atahakikisha anaunda Katiba yenye maoni ya wananchi na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuwaunganisha Watanzania dhidi ya ufisadi.
Mwanasiasa huyo mkongwe katika upinzani aliwaambia wafuasi wa CUF waliomsindikiza kuchukua fomu hiyo jijini hapa jana kuwa ameamua kuwania kiti hicho kwa mara ya tano kwa kuwa kati ya viongozi wa juu wa Ukawa anaamini ana sifa, uwezo, uadilifu, uwazi, uwajibikaji wa kuwaunganisha Watanzania ili waondokane na rushwa na ufisadi uliokithiri nchini.
Profesa Lipumba aliyekabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Mohamed Mkandu saa 6.55 mchana, alitaja vipaumbele vyake kuwa ni kujenga misingi ya kuhakikisha watoto wanapata fursa sawa ya maendeleo, ajira, afya, kulinda rasilimali za umma na kupambana na ufisadi.
Profesa Lipumba aliyeanza hotuba yake ya takriban dakika 45 kwa kutoa wasifu wa usomi na kazi mbalimbali za kiuchumi alizozifanya kwa takriban miaka 40, alisema anafahamu bayana matatizo mengi ya Watanzania kwa kuwa amezaliwa na kukulia kijijini.
Alisema matatizo hayo yamesababishwa na “siasa mbovu za chama cha mapinduzi” ukiwamo ufisadi, hivyo iwapo atapatiwa ridhaa ya kuwania kiti hicho cha juu, atakuwa na kazi kubwa ya kuleta uongozi makini utakaohakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa maendeleo ya watu wote.
Alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais, hatakuwa na msalie mtume na mafisadi na wote wanaohusika watawajibika kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Inatisha sana kuona mafisadi wakubwa, wala rushwa wakubwa badala ya kuwa ndani ya jela, wanachukua fomu za urais. Tunahitaji kwa kufuata taratibu na haki, mafisadi hao watumikie vifungo na mali zilirudishwe kwa umma walikofisadi,” alisema Profesa Lipumba huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Iwapo atapatiwa nafasi ya urais, alisema katika utawala wake atahakikisha watoto nchini wanapatiwa fursa sawa ya maendeleo kwa kutoa huduma bora afya, lishe na elimu.
Alisema suala la ukuaji imara kwa watoto halijapatiwa kipaumbele na kusababisha udumavu unaowanyima uwezo mkubwa wa kufikiri pindi wanapokuwa wakubwa.
Mwanasiasa huyo alisema anachukua fomu nchi ikiwa njia panda baada ya Katiba Inayopendekezwa kuacha masuala ya msingi ya uadilifu na uwajibikaji na kusababisha wachache kujinufaisha kwa rushwa.
MWANANCHI
 Chama cha ACT – Wazalendo kinatarajia kumtagaza mgombea wake wa urais wa Agosti 10, imefahamika.
Chama hicho kimesema mtia nia atakayepeperusha bendera ya ACT – Wazalendo atawajibika kutangaza mali binafsi na vyanzo vyake kwa kufuata utaratibu ulioanishwa katika katiba ya chama hicho.
Hayo yalisemwa jana mjini Geita na Kiongozi wa Chama hicho, Zitto Kabwe wakati akihutubia mamia ya wananchi katika viwanja vya Stand mjini hapa.
Alisema Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho iliyokutana juzi mjini Tabora, imepitisha ratiba kamili ya kuchukua na kurudisha fomu kwa nafasi mbalimbali za chama hicho kuanzia Julai Mosi.
“Kuanzia Julai Mosi mpaka Julai 17 ni kuchukua fomu kwa ngazi ya udiwani kwa ada ya Sh10,000, Julai 1-26 kuchukua fomu kwa ngazi ya ubunge na uwakilishi na ada yake ni Sh20,000 na kwa ngazi ya urais shughuli hiyo itakuwa kati ya Julai 1-26 na ada yake ni Sh100,000,” alisema Zitto na kuongeza:
“Vikao vya ngazi mbalimbali ya uteuzi vitaanza kuanzia Julai 27 hadi Agosti 10 mkutano mkuu wa chama utakapopitisha jina la mgombea urais.”
Zitto alisema lazima mgombea huyo awe amethibitika kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT – Wazalendo na aonyeshe utayari wa kuisimamia na kuiishi, awe ni mtu anayejitegemea kutokana na chanzo halali cha kipato kutokana na shughuli halali.
Alisema pia atakayetaka kukiwakilisha chama hicho kwa nafasi ya urais, itampasa kuwa mwenye haiba na taswira ya kuiwakilisha na kuipa heshima stahiki Tanzania katika Jumuiya za Kimataifa.
Chama hicho kinaendelea na ziara yake ya kulinadi azimio la Tabora lililozinduliwa juzi Mjini Tabora likilenga kuhuisha Azimio la Arusha. Leo watakuwa katika Mkoa wa Kagera.
MWANANCHI
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta jana alikamilisha mchakato wa kusaka wadhamini wa maombi yake ya kuwania urais kupitia CCM na leo anatarajia kuwa wa kwanza kurejesha fomu hizo makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma.
Sitta ambaye ni miongoni mwa wanaCCM 32 waliokwishachukua fomu kuwania nafasi hiyo, atarejesha fomu hizo baada ya kupata saini za wanaCCM katika mikoa 21 nchini. Kila mgombea anatakiwa kupata wadhamini 450 katika mikoa 15, kati ya hiyo mitatu ya Zanzibar.
Akizungumza na wakazi wa Itundu na mjini Urambo alikomalizia mzunguko huo, Sitta alisema kazi ya urais si lelemama ila ataimudu kwani anaifahamu vizuri nchi.
Alisema endapo atateuliwa na chama chake kugombea urais na kushinda ataimarisha Muungano na kupambana na ufisadi na uonevu kwa wananchi ili kila mtu afurahie maisha yake.
Aliahidi kuiimarisha CCM kiuchumi ili isiyumbishwe na matajiri.
NIPASHE
Wakati makada wa Chama Cha Mapindizi (CCM) wakiendelea kumiminika kuchukua fomu ya kuomba chama chao kiwateue kuwania urais, imebainika kuwa mawaziri 12 wa serikali ya sasa ya Rais Jakaya Kikwete wamejitosa kuwania nafasi hiyo na kuipiku rekodi ya mawaziri wa serikali ya Rais Benjamin Mkapa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Idadi hiyo (ya mawaziri 12) imefikiwa baada ya kujitokeza pia kwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha Rose Migiro, ambaye ratiba inaonyesha kuwa atachukua fomu leo makao makuu ya CCM mjini Dodoma.
Ofisa Habari CCM makao makuu, Gabriel Athuman, jana alisema Dk. Migiro atachukua fomu saa 4:00 asubuhi, sawa na kada mwingine aitwaye Salum Maluku na hivyo kufanya idadi ya makada wote waliojitokeza kuwania urais kufikia 33.
Idadi iliyofikiwa sasa ya mawaziri wanaowania kuteuliwa na CCM ili wachuane na wapinzani katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu kwa nia ya kumrithi Rais Kikwete inaipiku idadi ya mawaziri waliojitokeza kumrithi Mkapa katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2005, ambao mawaziri waliochuana zaidi na kufika mbali katika harakati za kuwania nafasi hiyo walikuwa wanne tu.
Mawaziri waliochukua fomu ya urais mwaka 2005 na kuchuana vikali ndani ya mchujo wa CCM walikuwa ni Rais Kikwete aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri Mkuu (mstaafu), Frederick Sumaye.
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji, Dk. Abdallah Kigoda (sasa Waziri wa Viwanda na Biashara) na Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Prof. Mark Mwandosya (sasa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalum).
Mbali na Migiro, mawaziri wengine waliochukua fomu kutaka kumrithi Rais Kikwete hadi kufikia leo ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta; Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira na Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titus Kamani.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi Maalum, Prof. Mwandosya; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Mawaziri wengine ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Katika hatua nyingine, inaelezwa kuwa Kamati Kuu ya Chama hicho itakayokutana Julai 12 itakuwa na kibarua cha ziada katika kuwachuja wagombea na kubaki na majina ya kuyapeleka mbele ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutokana na ukweli kuwa baadhi ya waliojitokeza ni wajumbe pia wa CC, baadhi wakitokana na nyadhifa zao.
Hao ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal ambaye pia ameshachukua fomu kuwania urais, Waziri Mkuu Pinda, Wasira na Migiro.
NIPASHE
Wakati utoaji huduma za afya ukizidi kuzorota katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ukosefu wa damu umekuwa tatizo sugu linalosababisha mateso na vifo kwa wagonjwa.
Hospitali hiyo inahitaji wastani wa chupa za damu 70 hadi 100 kwa siku kwa ajili ya kuwawekea wagonjwa mbalimbali, lakini imekuwa na uwezo wa kupata chupa 20 hadi 30 pekee kwa siku.
Baadhi ya madaktari wa hospitali hiyo waliliambia NIPASHE kuwa ukosefu wa damu MNH ni wa muda mrefu, hivyo `kujenga’ mazingira ya kuamini kuwa uongozi wake umeshindwa kulipatia ufumbuzi wa kudumu.
Daktari bingwa wa watoto hospitalini hapo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema ni kawaida kwa wagonjwa wanaohitaji damu kukaa wodini hadi siku tatu na wengine kufa kutokana na kukosa damu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, baadhi ya wagonjwa wanawekewa damu kidogo ya mahitaji kama sharti la kuwashirikisha ndugu, jamaa na marafiki kuchangia, na inapotokea wasijitokeze kufanya hivyo, madaktari wanasitisha kumuongezea (mgonjwa) damu iliyobaki.
Lengo la hatua hiyo linaelezwa kuwa ni hamasa kwa walio karibu na mgonjwa kuchangia ili irejeshwe kwenye benki ya damu kwa vile wakati mwingine, damu inayotolewa inaweza isiwe kundi la ile inayohitajika kwa mgonjwa.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa inapotokea dharura kwa mgonjwa kuhitaji damu, MNH inamkopesha (mgonjwa) kiasi kidogo cha damu kuokoa maisha kwa wakati husika, huku ndugu wakitakiwa kuchangia ili kufidia kiasi halisi kinachohitajika.
“Kama mtu amezidiwa wakaona anaweza kufa, wanamkopesha damu kidogo kama unit moja ambayo ni nusu lita na haitoshi, lakini lengo ni kuwalazimisha ndugu wa mgonjwa kuchangia kiasi cha damu inayohitajika,” kilieleza chanzo kingine katika wodi ya wanawake.
Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya vifo vikiwamo vinavyotokea kwenye wodi vinahusishwa na ukosefu wa damu.
Taarifa za kitabibu kutoka kwa madaktari wakiwamo wa MNH zinaeleza kuwa mgonjwa anayehitaji kuongezewa damu akikaa muda mrefu bila kupata huduma hiyo, moyo unashindwa kufanya kazi na hivyo kusababisha kifo.
Vyanzo tofauti vimebaini kuwa uongozi wa MNH unalaumiwa kwa hali hiyo kutokana na kushindwa kukusanya damu kwa wingi kwani hakuna jitihada zozote zinazofanyika kama vile kuhamasisha wananchi kujitolea damu kwenye kitengo cha damu.
Watu wanaoathirika kutokana na ukosefu wa damu ni wanaofanyiwa upasuaji, wenye matatizo yanayohusiana na tumbo, wanaoharisha na kutapika damu, wenye saratani ya damu, upungufu wa damu na magonjwa ya kuambukiza.
Daktari anayezungumza na NIPASHE kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, alisema upungufu wa damu unasababishwa na uzembe wa kitengo cha damu kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo kama kuhakikisha kunakuwa na akiba ya damu ya kutosha, hivyo kuweka rehani maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu.
Wakati MNH ikidaiwa kushindwa kufanikisha upatikanaji damu, mwamko wa umma bado ni mdogo katika kutoa damu inayohitajika kwa maisha ya wagonjwa.
HABARILEO
Shule ya Msingi Saadani Chumvi iliyopo Kata ya Mkange wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, imefungwa baada ya wazazi kuwa na hofu baada ya watu wawili na mbuzi 70 kuliwa na Simba kutoka kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Shule hiyo ambayo iko jirani na hifadhi hiyo ilifungwa mwishoni mwa mwaka jana kutokana na matukio hayo hali ambayo ilisababisha wazazi kuogopa watoto wao kudhuriwa na wanyama hao hivyo kuwahamishia watoto wao kwenye shule ya Msingi ya Saadani.
Akizungumza jana, Mtendaji wa Kijiji cha Saadani, Hussein Msilu alisema mara baada ya matukio hayo wazazi wa watoto hao waliingia hofu na kuwaondoa watoto wao wapatao 67 na kuwahamishia kwenye shule hiyo ya Saadani ambayo iko umbali wa kilomita kati ya sita na saba.
Msilu alisema kutokana na hali hiyo uongozi wa kata na kamati ya shule kwa pamoja walikubaliana wanafunzi hao kuhamishiwa kwenye Shule ya Msingi Saadani kutokana na hofu iliyotanda kuwa wanafunzi wanaweza kuliwa na simba hao.
Alisema wanaushukuru uongozi wa kiwanda cha chumvi kwa kutoa usafiri kwa ajili ya kuwasafirisha wanafunzi kwenda na kurudi kutoka kwenye Kitongoji hicho cha Saadani Chumvi hadi shuleni Saadani, kwani umbali ulikuwa mrefu sana pia ni hatari kwani wanapita ndani ya hifadhi hiyo ambayo ina wanyama mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete alisema alipata taarifa hiyo na kuwasiliana na mamlaka husika na kwamba tayari zilichukuliwa za kuwaondoa simba hao, lakini kilichobaki kwa sasa ni hofu ya wananchi.
Aidha, aliwatoa hofu wazazi na kuwaambia wawarejeshe watoto hao shuleni hapo ili waendelee kusoma hapo kwani ni karibu na makazi yao tofauti na Saadani ambako ni mbali pia ni usumbufu mkubwa kwao, kwani hali hiyo imedhibitiwa.
MTANZANIA
Mahakama Kuu yaAfrika Kusini imetoa amri ya muda ya kumzuia Rais wa Sudan, Omar al Bashir anayehudhuria kikao kilichoanza jana cha viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) kutoondoka nchini humo.
Mahakama hiyo imemuagiza al-Bashir abakie hadi leo wakati itakaposikiliza kesi inayoitaka iiamrishe Serikali ya Afrika Kusini kumkamata kiongozi huyo i akajibu mashitaka yanayomkabili katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) ya mjini Hague, Uholanzi.
Mapema jana, Rais Bashir alikaribishwa na maofisa wa Afrika Kusini wakati akiwasili mjini Johannesburg.
Licha ya a mahakama kutangaza uamuzi huo, kiongozi huyo wa Sudan alipiga picha ya pamoja na viongozi wengine wa Afrika akiwa amevalia suti ya bluu, tai na akitabasamu wakati picha ikichukuliwa.
Rais al Bashir anasakwa na mahakama hiyo kwa uhalifu wa vita na mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.
AU inakutana chini ya uenyekiti wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe katika mkutano unaoonekana kughubikwa na mzozo wa Burundi na migogoro ya uhamiaji, ugaidi na mihula mitatu ya urais.
AU imekuwa ikikiuka maombi kadhaa ya kuitaka imkamate al- Bashir tangu amri hiyo mkamata ilipotolewa mwaka 2009.
Hali hiyo imezusha mvutano baina ya ICC na AU huku baadhi barani Afrika wakiituhumu mahakama hiyo kuwa chombo cha kuwalenga Waafrika tu.
Hata kabla ya matukio ya jana, AU imekuwa ikiitaka ICC iache kuwaandama marais walio madarakani na kwamba haitalazimisha wanachama wake kumkamata kiongozi yeyote kwa niaba ya mahakama hiyo.
Chama tawala cha African National Congress (ANC), kilisema Serikali ya Afrika Kusini ilitoa msamaha ‘kwa washiriki wote wa mkutano wa wa AU kama sehemu ya taratibu za kimataifa kwa nchi wenyeji wakati wa mikusanyiko ya AU au hata Umoja wa Mataifa (UN).
“Ni katika msingi huu, pamoja na mambo mengine ANC inatoa mwito kwa Serikali ya Afrika Kusini kupinga agizo hilo lililoletwa kuilazimisha kumkamata Rais al-Bashir,” taarifa ya ANC ilisema na kuongeza kuwa mataifa ya Afrika na Ulaya Mashariki yanaendelea kukandamizwa kwa kulengwa isivyo halali na uamuzi wa ICC.
Lakini kwenye taarifa yake , ICC ilisema kuwa waranti mbili za kumkamata Bashir bado zipo. Mwendesha Mashitaka wa ICC, Fatou Bensouda amesema Afrika Kusini ina wajibu wa kumkamata al-Bashir na kumkabidhi kwa mahakama hiyo.
Ofisi yake imekuwa ikiwasiliana na mamlaka za Afrika Kusini tangu iliporipotiwa kuwa rais huyo wa Sudan atazuru nchi hiyo kuhudhuria mkutano wa AU.
Iwapo al-Bashir hatakamatwa, suala hilo litawasilishwa kwa mkutano wa mataifa wanachama wa mahakama hiyo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo liliiwasilisha kesi hiyo ICC mwaka 2005, alisema.
Al-Bashir, aliyeingia madarakani kwa mapinduzi mwaka 1989, anatuhumiwa kutenda uhalifu ambao pamoja na mambo mengine umeshuhudia vifo vya watu 300,000 na wengine milioni mbili kukimbia makazi yao.
Hati za kumkamata Bashir, ambaye amekana tuhuma zinazomkabili, zimemfanya anatembelea nchi chache duniani, hasa mataifa rafiki ya Afrika na Mashariki ya Kati.

0 comments:

Post a Comment