Thursday, May 23, 2013

GHASIA KUBWA ZA MTWARA


mtwara 6104f
Vurugu hizo zilitokana na hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kusisitiza kuwa bomba la gesi kutoka Mtwara na kuja Dar es Salaam litajengwa, jambo lingine linalodaiwa kusababisha ghasia hizo ni hatua ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kutokurusha moja kwa moja matangazo ya Bunge hivyo kuwakosesha wananchi fursa ya kusikiliza bajeti hiyo.

 Hali ya usalama mkoani Mtwara ni tete. Mtu mmoja anaaminika kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kutokana na vurugu kubwa zilizozuka jana huko Mtwara baada ya kusomwa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Madini na Nishati bungeni Dodoma jana.
Aidha, askari wanne wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wamefariki dunia katika ajali wakitokea Nachingwea kwenda Mtwara ili kusaidia kutuliza vurugu hizo. Katika ajali hiyo, askari 20 walijeruhiwa, wengi wao vibaya na saba walinusurika.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Dk Mohamed Kodi alithibitisha kupokea maiti moja na kuomba apewe muda kutaja idadi ya majeruhi.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alidai kwamba hakuna mtu aliyefariki dunia wala majeruhi. Alisema watu 45 wamekamatwa.
Milio ya risasi za moto na mabomu ya machozi vilisikika kila kona na hasa Mitaa ya Mdenga, Magomeni na Shengena Mjini Mtwara ambako hali ilikuwa mbaya kutokana na kuwapo kwa mapambano kati ya polisi na vijana.
Vurugu hizo zilitokana na hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kusisitiza kuwa bomba la gesi kutoka Mtwara na kuja Dar es Salaam litajengwa, jambo lingine linalodaiwa kusababisha ghasia hizo ni hatua ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kutokurusha moja kwa moja matangazo ya Bunge hivyo kuwakosesha wananchi fursa ya kusikiliza bajeti hiyo.
Akizungumzia kukosekana kwa matangazo hayo ya televisheni, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Clement Mshana alisema kukatika kwa matangazo hayo kulitokana na tatizo la satelaiti katika mji huo na Musoma.
Hata hivyo, wakazi wa Mtwara waliokuwa na ving'amuzi walipata fursa ya kuangalia matangazo hayo.
Pia vurugu hizo zilichangiwa na vipeperushi vilivyosambazwa na watu wasiojulikana wakitaka watu kuacha kufanya shughuli zozote na kukaa nyumbani ili kufahamu hatima ya mradi wa usafirishaji wa gesi kutoka Msimbati hadi Dar es Salaam kwa njia ya bomba.
Katika vurugu hizo zilizozagaa zaidi maeneo ya Mikindani na Magomeni, wananchi pia waliharibu Daraja la Mikindani linalounganisha Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.
Tangu asubuhi kama ilivyokuwa Mei, 17 mwaka huu, Mji wa Mtwara ulikuwa kimya na huduma nyingi za kijamii zilisimama ikiwamo usafiri wa pikipiki, daladala, mabasi maduka na masoko.
Katika Mtaa wa Magomeni, nyumba ya Mwandishi wa TBC, Kassim Mikongolo iliteketezwa kabisa kwa moto na kundi hilo la vijana. Pia nyumba za Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnein Murji na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi) ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia zilichomwa moto.
Mikongolo alisema nyumba yake ilichomwa moto saa nne asubuhi... "Walipania kuchoma nyumba yangu kwa kuwa mke wangu ni Koplo wa Jeshi la Polisi."
Katika Mtaa wa Majengo, kundi la vijana lilivamia Ofisi ya CCM Kata na Ofisi ya Serikali ya Kata na kuanza kuzibomoa. Pia nyumba ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mtwara-Mikindani, Ali Chinkawene ilirushiwa mawe.
Ofisi ya Mtendaji Mtaa wa Msikitini, Kata ya Reli na Ofisi ya CCM Chikongola nazo zimeteketezwa kwa moto. Wanafunzi wa Shule za Msingi Shangani na Majengo walirejeshwa nyumbani baada ya mabomu ya machozi kurindima kuanzia asubuhi hadi mchana.
"Ni kweli Ofisi ya CCM na Ofisi ya Serikali ya Kata zimebomolewa, nyumba yangu imerushiwa mawe," alisema Chinkawene kwa sauti ya chini na kukata simu.
Msimbati shwari
Wakati Mtwara Mjini hali ikiwa tete, katika Kijiji cha Msimbati ambako gesi asilia inachimbwa, hali ni shwari na wananchi walikuwa wanaendelea na kazi zao kama kawaida.
"Maduka na soko vimefunguliwa, huku hali ikiwa shwari kabisa ingawa msimamo wetu upo palpale, hatutaki gesi iende Dar es Salaam kwa njia ya bomba," alisema mkazi wa kijiji hicho, Juma Ayoub.
JWTZ wafariki ajalini
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mtwara, Edward Gontako alithibitisha kutokea ajali hiyo ya askari wa JWTZ, 41KJ Nachingwea na kusema wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Wilaya, Dk John Sijaona alithibitisha kupokea maiti za askari hao na kusema hali za majeruhi ni mbaya na kwamba mipango ilikuwa inafanywa kuwapeleka katika Hospitali ya Ndanda, Mtwara.

0 comments:

Post a Comment