Saturday, July 20, 2013

WEMA SEPETU KUPANDA KIZIMBANI



KUNA kila dalili kwamba mrembo anayetamba kwenye filamu za Kibongo, Wema Isaac Sepetu jela inamwita na anatakiwa kufanya maombi ili kukwepa kifungo maishani mwake.

Hali hiyo inafuatia staa huyo kupandishwa kizimbani kwa mara nyingine tena Jumatano iliyopita, pale alipopanda katika Mahakama ya Mwanzo ya Kawe jijini Dar kwa kosa la kumpiga na kumtukana matusi ya nguoni meneja wa hoteli moja iliyopo Kawe Beach jijini Dar, Godluck Kayumbu.



Kabla ya kupandishwa kwa ‘pilato’, staa huyo anayemiliki Kampuni ya Endless Fame alikuwa akisakwa na askari kwa siku kadhaa na kufanikiwa kuwapiga chenga za hapa na pale.

Hata hivyo, mbio zake ziliishia ukingoni Julai 16, mwaka huu, alipokamatwa saa mbili usiku akiwa anafuturu na wageni wake nyumbani kwake, Kijitonyama Dar.


Askari saba walifika nyumbani kwake wakiwa ndani ya Land Rover ‘difenda’ kwa ajili ya kumkamata, hata hivyo walipata upinzani kidogo kutoka kwa mlinzi wa staa huyo ambaye alikuwa akizuia bosi wake asikamatwe ambapo ilibidi askari hao wakaze msuli na kutuliza mtiti uliokuwa ukitaka kutokea.

Baada askari kumfikia staa huyo, walimtaka kwenda naye kituo cha polisi kwa kutumia difenda walilofika nalo ambapo Wema alipinga na kugeuka mbogo kwa kudai kwamba hawezi kupanda difenda kutokana na hadhi yake.

Pamoja na askari kutaka kumpandisha kwa nguvu, staa huyo alipinga na ikakubaliwa apande gari lake aina ya Audi Q7 huku akiwa chini ya ulinzi wa askari.

Safari ikaishia Kituo cha Polisi cha Kawe ambako staa huyo aliandikisha maelezo na baada ya zoezi hilo akatupwa selo.


Kama lilivyo jina lake, wema hauozi, staa huyo alipata dhamana saa 5 za usiku baada ya kudhaminiwa na msanii mwenzake wa filamu, Kajala Masanja.

Kajala aliwahi kutolewa katika mdomo wa jela na Wema siku za nyuma baada ya kukutwa na hatia na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar alipotakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 13 au kwenda jela, Wema alimlipia kiasi hicho cha fedha.

Wapambe wa Wema waliokuwa wamejazana nje ya kituo hicho cha polisi, walilipuka kwa shangwe baada ya bosi wao kuchomolewa kutoka selo. Staa huyo aliondoka na gari lake lililokuwa likiendeshwa na meneja wa kampuni yake aitwaye Petit Man.
Julai 17, asubuhi Wema alirudi kituoni hapo na kuwekwa chini ya ulinzi kwa ajili ya kupelekwa mahakamani kusomewa mashitaka yake.

Katika hatua ya kushangaza, staa huyo alitembezwa kwa miguu umbali wa mita 200 kutoka kituo cha polisi hadi Mahakama ya Mwanzo ya Kawe.

Wema alipandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka yake na Mh. Hakimu, Bernice Ikanda na kudaiwa kufanya vurugu, kushambulia kwa kumpiga makofi na kumtukana Kayumbu.
Mbele ya hakimu, Wema alikana mashitaka na hakimu aliiahirisha kesi hiyo mpaka Julai 31, mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment