Home »
» IDADI WA UFAULU WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA NNE YA ONGEZEKA NA MATOKEO YA KIDATO CHA SITA YAKO TAYARI
|
KATIBU MTENDAJI WA NECTA Dk. JOYCE NDALICHAKO |
Dar
es Salaam. Idadi ya watahiniwa waliofaulu mtihani wa kidato cha nne
mwaka jana imeongezeka kwa kati ya asilimia 20 na 23 baada ya Baraza la
Mitihani la Taifa (Necta), kufanya marekebisho alama za viwango vya
ufaulu, Mwananchi limebaini.
Habari ambazo gazeti
hili imezipata zinasema matokeo hayo ambayo yamewezesha kiwango cha
ufaulu kupanda na kufikia asilimia kati ya 54 na 57, huenda yakatangazwa
wiki hii pamoja na yale ya kidato cha sita ambayo pia yamechelewa
kutangazwa.
Chanzo cha habari
kutoka Necta kimesema matokeo hayo mapya yanaonyesha kuwa, ufaulu wa
kuanzia daraja la kwanza hadi la nne umeongezeka kutoka asilimia 34.5
kwa matokeo yaliyotangazwa awali na huenda yakafikia asilimia 57.
Hii
inamaanisha kwamba watahiniwa wapatao 82,000 ambao awali walikuwa
wamepata sifuri katika matokeo ya awali sasa wamepanda na kupata
madaraja ya ufaulu katika matokeo mapya.
Kwa matokeo hayo, watahiniwa wa mwaka 2012 watakuwa wamefanya vizuri
kuliko wa mwaka 2011, ambao watahiniwa 225,126 sawa na asilimia 53.37 ya
349,390 waliofanya mtihani huo walifaulu.
Msemaji wa Necta, John Nchimbi alisema upangaji wa matokeo hayo ulikuwa
bado unaendelea.
“Ninachojua kwa
sasa ni kuwa mchakato unaendelea na matokeo yatatangazwa mapema tu ili
watoto waweze kujiunga na shule mapema,” alisema Nchimbi.
Pia alisema usahihishaji wa mitihani ya kidato cha sita umekamilika.
Matokeo ya awali
Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Dk Shukuru Kawambwa yalionyesha kuwa kati ya watahiniwa 367,756
waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, waliokuwa wamefaulu kwa
daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa 126,847 sawa na asilimia 6.4.
Waliopata daraja la nne walikuwa ni 103,327 sawa na asilimia 28.1.
Katika matokeo hayo, watahiniwa 240,909 sawa na asilimia 65.5 walipata
sifuri, hesabu ambayo imebadilika katika matokeo mapya ambayo
yanaonyesha kuwa sasa waliopata daraja hilo ni 158,100 ambayo ni
asilimia 43.
Hata hivyo, habari kutoka Necta zinasema kuwa licha
ya kuwezesha kuongezeka kwa waliofaulu, matumizi ya kanuni mpya ya
kukokotoa matokeo hayo yalisababisha zaidi ya wanafunzi 2,500 kushuka
ufaulu ikilinganishwa na awali. Maofisa mbalimbali wa Necta pamoja na
wale wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na taasisi zake, walikutana
mwishoni mwa wiki iliyopita kukubaliana masuala mbalimbali juu ya
matokeo hayo pamoja na suala la matokeo ya wanafunzi hao 2,500 kabla ya
kutangazwa wiki hii.
“Baada ya wajumbe kujadili suala lile, busara ilibidi itumike kwa hiyo
hakuna mwanafunzi ambaye alama yake itashuka, kwa kawaida isingewezekana
mtoto ambaye matokeo yalitoka akiwa amefaulu leo umwambie ameshuka,”
kilieleza chanzo chetu.
0 comments:
Post a Comment